Sunday, August 26, 2012

Rooney Anaweza Uzwa £50m Kama Hatojirekebisha, Ferguson Aongea

Wayne Rooney jana alipata jeraha kubwa kwenye paja lake la kulia -  na anaweza kuuzwa kwa pauni milioni 50 kama hatarekebisha mwenendo wake wa maisha.
Maneno ya Sir Alex Ferguson nayo yanazidi kuchochea wasiwasi uliotanda juu ya hatma ya Wayne Rooney.

Gezeti la The Sun linaripoti juu ya ustahamilivu wa Manchester United kwa Wayne Rooney unavyozidi kuzorota. Inavyoonekana usajili uliofanyika umewaongezea jeuri Man U kutokukubali tena kupelekeshwa na tabia za Rooney kama ilivyokuwa awali.

Kwa sasa United wanafikiria kumuuza kwa pauni milioni 50 kama hawataona mabadiliko katika tabia zake kwa ujumla. Jana Rooney alikimbizwa hospitali - swali la msingi je atarudi?

Alex Ferguson hawajahi sema kitu bila kuwa na sababu iliyojificha, jana alipoulizwa juu ya van Persie alimsifu kwa anavyoonesha ana mapenzi na United na anataka kuwa Old Trafford.

Alisema: " Nawaheshimu sana wachezaji wanaotaka kuchezea timu yetu. Na hicho ndicho hunivutia kwa mchezaji pindi napotaka kuamua nani nimnunue.
Kinyume cheke hua kinyume pia, kama nasikia mchezaji hana mapenzi tena na sisi na anataka kuhama basi nitamsaidia kumtoa nje ya mlango."

Rooney mwezi Oktoba 2010, alisema United hawana tena mshawasha wa kushinda vikombe na akatamka anataka kuihama timu hiyo. Ferguson hawawahi kufanyiwa hivyo na mchezaji yoyote katika maisha yake ya soka. 

Na kufanya hali kuwa mbaya zaidi si tu lilibaki lisaa limoja Rooney kuihama United bali kujiunga na mahasimu wao wakubwa Manchester City.

Sakata hilo litonesha kidonda ambacho kilikua hakijapona. Fergie ilibidi ambembeleze Rooney abadili mawazo kwa sababu hakutaka kuidhoofisha United kwa faida ya Man City.

Msimu huo Rooney alikuwa mmoja kati ya washambuliaji bora duniani akifunga magoli ya kila aina. Ila hayo hayawezi kusemwa sasa: mchezo dhidi ya Everton siku ya Jumatatu ulionesha si Rooney yule tunayemjua sisi na Ferguson analijua hilo.
Na kipengele cha maneno ya Ferguson ni: "mchezaji hana mapenzi tena na sisi" ndio kinaingia hapa.

Rooney hakuingizwa mpaka ilipofika dakika ya 68 katika ushindi wa 3-2 dhidi ya Fulham Old Trafford - na haikuwa siku yake kwani ilibidi abebwe kwenye machela baada ya kuchanika paja katika muda wa nyongeza.
Rooney akipewa huduma ya kwanza jana
Ni dhahiri kwa sasa Robin van Persie, ambaye alifunga goli lake la kwanza kwa United hapo jana, ndiye atakua mshambuliaji namba moja kwa Ferguson.
Na, hata akirudi kwenye fomu, itabidi apiganie namba na wengine ya kumlisha van Persie.

Ferguson hajawahi kusita kumuacha mchezaji mwenye jina kubwa kama atahisi ameshuka kiwango ama hamsikilizi tena.

Kama Rooney kasahau basi awaulize: Jaap Stam, Ruud van Nistelrooy, Devid Beckham na Roy Kean. Rooney anaonekana mzito na mshawasha aliokuwa nao kila anapoichezea United unaoneka kufifia, pia anaonekana mwenye uchovu na mawazo.

Lakini Fergie hawezi kutoa maamuzi kwa kuangalia mechi moja, ila Rooney hajafikia hali hii kwa bahati mbaya bali ni kwa kufanya vitu alivyokuwa akikatazwa na Ferguson mara kwa mara.  

Inasemekana Ferguson ana kisirani na Rooney na hajaongea naye tokea kurudi kwenye mechi za matayarisho. Kikao kilifanyika mapema mwezi huu kati ya Fergie na bodi ya United kujadili mwenendo wa tabia za Rooney na athari zake kwa klabu.

Vitu vilivyojadiliwa ni pamoja na picha zilizomuonesha Rooney akilewa na kuvuta sigara hadharani ilhali akiwa ni kioo cha United hivyo kuathiri makubaliano ya mikataba ya kibiashara waliyoingia United  inayowataka wachezaji wawe mifano kwa jamii.

Alichaguliwa kuwa mwanasoka bora wa Uingereza May 2010, kutokana na mambo aliyoyafanya nje ya kiwanja, alivurunda vibaya Kombe la Dunia lililofanyika kusini mwa bara la Afrika.

Mwezi August mwaka 2010, alipigwa picha zingine tena akiwa anavuta sigara na kujisaidia haja ndogo hadharani nje ya klabu ya usiku Manchester.

Kwa hapa Tanzania tunaweza ona ni kosa dogo ila kwa Ulaya hua ni kosa kubwa sana na huaribu taswira ya timu na biashara za klabu kwa ujumla.
Rooney baada ya kuumia akisubiri huduma ya kwanza 
Mwezi Septemba stori za maisha yake binafsi juu ya kuwa na mahusiano nje ya ndoa yaliathiri mwenendo mzima wa United katika kampeni yao ya kulitwaa kombe la ligi kuu ya Uingereza. 

Ferguson ilibidi amuondoe kikosini dhidi ya timu yake ya utotoni Everton kuhofia angecheza chini ya kiwango kwa kujua atazomewa sana na mashabiki pinzani hivyo angepoteza umakini.

Ferguson alimuondoa pia kwenye michezo dhidi ya Valencia na Sunderland, akimtetea kuwa na maumivu ya kifundo cha mguu, kwa jeuri Rooney aliviambia vyombo vya habari Ferguson hakusema kweli na ye ni mzima wa afya.

Wakati watu wakijiuliza jeuri hiyo Rooney kaitoa wapi! Akatoboa: NATAKA KUHAMA.
Baadae alibadili mawazo ila shutma alizotoa juu ya United ziliwachoma sana na bado mpaka sasa ni donda.

Jambo la faraja kwa mwaka huo lilikua kwamba Man U walichukua kombe na kufika fainali ya Champions League. 

Ila Rooney aliendelea kumuudhi Ferguson. Baada ya ushindi wa 4-0 dhidi ya Wigan siku ya Boxing Day msimu uliopita.

Ferguson aliwaambia wachezaji wote wapumzike majubani mwao na wasionekane hadharani kwa kuwa siku inayofuata hapatakuwa na mapumziko na wana mazoezi muhimu, wote walifuaa ila Rooney alitoka!

Siku iliyofuata mazoezini alikua mzito kwa kila jambo -  Ferguson kwa hasira alimpiga faini ya pauni 250,000. Kwa kushindwa kufanya mazoezi ilibidi amuondoe kwenye kikosi kilichocheza siku ya mkesha wa mwaka mpya dhidi ya Blackburn, mchezo huo walipoteza.

Msimu uliisha bila kombe lolote, huku Rooney akitikisa nyavu mara 34, kwa hili magoli yake hayakuwa na maana kwa Ferguson, ila ikatafsiriwa kama tabia zake ziliathiri kikosi kizima cha United kupoteza michezo iliyoonekana rahisi.

Euro 2012 ikaja haraka, kama ilivyo desturi yake kwenye mashindano makubwa alicheza tena chini ya kiwango, akikosa mechi mbili za kwanza kwa kadi nyekundu aliyooneshwa kizembe kwa kosa la kumpiga teke mchezaji wa Montenegro akiwa hana mpira.

Sasa angalau utakuwa unajua sababu na haitokuja kama mshangao ukisikia Rooney anauzwa.
Tunamtakia Rooney apone haraka baada ya kuchanika paja hapo jana, na kama anataka kuokoa maisha yake ya Old Trafford basi inabidi akiwa hukohuko hospitali aanze kubadilika.

Holla, nice weekend!!!!!!!!!!!!

No comments:

Post a Comment